FAHAMU ZAIDI KUHUSU FISTULA
Fistula ni njia isiyo ya kawaida inayounganisha uke na njia ya mkojo au uke na njia ya haja kubwa au vyote kwa pamoja hivyo kuruhusu mkojo au haja kubwa kutoka kupitia kuta za uke bila kujizuia.
Kila mwaka wanawake 50,000 mpaka 100,000 huathirika na fistula ulimwenguni.~WHO
Visababishi vya fistula baada ya kujifungua ni nini?
Tatizo la fistula baada ya kujifungua hutokea Zaidi baada ya mwanamke mjamzito kuwa katika hali ya uchungu kwa muda mrefu(prolonged and obstructed labor) hali ambayo huweza kutokana na kichwa cha mtoto kushindwa kupita kutokana na njia kuwa ndogo (huweza kutokana na umri mdogo wa mwanamke pia) kuliko ukubwa wa kichwa.
Kushindwa kupita kwa kichwa cha mtoto na kuwa katika hali ya uchungu kwa muda mrefu hupelekea kichwa kugandamiza tishu za uke, kibofu na njia ya haja kubwa hivyo kupelekea tishu hizi kukosa damu, kukosa damu kwa tishu hizi hupelekea uharibifu kwenye tishu hizi na kusababisha tundu kutokea kati ya uke na kibofu cha mkojo au kati ya uke na njia ya haja kubwa hivyo kusababisha mwanamke kutoka mkojo au haja kubwa bila kujizuia.
Wataalam wa afya pia wanaeleza kuwa fistula hutokea mara nyingi kwa wanawake wanaojifungulia majumbani ambako hukosa Huduma za matibabu.
Pia wakati mwingine huweza kuwa ni matokeo ya kujifungua kwa njia ya upasuaji, ajali au saratani ya maeneo ya nyonga.
Athari za tatizo la fistula.
Tatizo la fistula linakera na kuaibisha kwa sababu kutoka kwa haja kubwa au ndogo bila kujizuia husababisha harufu kali kwa mwathirika na jamii inayomzunguka hivyo kupelekea mwathirika kunyanyapaliwa na kutengwa na wanafamilia na jamii. Lakini pia tatizo hili huweza kuambatana na hatari zifuatazo kwa afya ya mwanamke;
-Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) -Matatizo ya usafi -Kuwashwa kwa Ngozi ya kuta za uke -Kutoka majipu -Maumivu makali wakati wa tendo la ndoa
Namna gani tunaweza kupunguza tatizo la fistula?
Tatizo la fistula linaweza kuzuilika.~WHO
Njia zifuatazo zikizingatiwa vyema huweza mara nyingi kuzuia tatizo la fistula baada ya kujifungua.
Kuhakikisha kuwa mwanamke anapata ujauzito wa kwanza akiwa amepevuka vyema.Kuacha tamaduni na desturi potofu kama vile kuzaa watoto wengi kama njia ya kuonyesha ufahari.Kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito na kujifungulia hospitali au kituo cha afya.Hatua stahiki kuchukuliwa inapotokea dharura kama vile kupata uchungu muda mrefu wakati wa kujifungua.
Matibabu ya fistula
Zaidi ya wanawake milioni mbili barani Afrika na Asia wanaishi na tatizo la fistula ambalo linaweza kutibika.~WHO
Tatizo la fistula linatibika kabisa hivyo basi unapopata tatizo hili la fistula usisite kwenda katika kituo cha afya kilicho karibu nawe uweze kupata maelekezo juu ya utaratibu uliowekwa na serikali kupitia wizara ya afya ikishirikiana na hospitali ya CCBRT na hospitali nyingine za serikali wa kupata matibabu ambayo hutolewa bure kwa sasa.

Comments
Post a Comment